Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar
VYAMA vya siasa 18, kati ya 19, vimetia saini fomu za maadili kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofannyika Oktoba 29, mwaka huu huku CHADEMA, hakikufanya hivyo.
Utiaji saini huo, umefanyika pamoja na uzinduzi wa nembo ya uchaguzi mkuu mwaka huu.
Akizungumza mjini Unguja, jana, baada ya kumalizika kwa utiaji saini, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, alivitaka vyama vya siasa, kuhakikisha vinaheshimu na kufuata maelekezo ya sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa uchaguzi.
Mwenyekiti huyo, alisema ni wajibu wa kila mdau katika kanuni hizo hasa vyama vya siasa, kulinda hali ya usalama, utulivu na amani ya Zanzibar.
Jaji Kazi, alisema vyama vinatakiwa kuhakikisha kunakuwa na ushiriki huru na ulinzi wa haki za makundi maalumu, kuheshimu na kufuata kikamilifu maelekezo ya sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa Jaji Kazi, vyama vinatakiwa kulinda utu, thamani na haki ya kuishi kwa kuheshimu haki ya kila chama, wanachama, wafuasi wa kila chama na wagombea wote wa uchaguzi, wakiwemo wanawake na wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi.
Aliwasisitiza kuheshimu kipindi cha kufanya kampeni kupitia mikutano ya hadhara, maandamano au misafara ya vyombo vya moto.
Mwenyekiti huyo, alisema katika kanuni hizo, tume inawajibika kufuata katiba, sheria na kanuni zinazoiongoza na kutopendelea chama cha siasa au mgombea na kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa sheria.
Kwa upande wa serikali, kanuni za maadili, zinatoa wajibu ikiwa ni pamoja na kutoa huduma na nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa bila ya upendeleo wa aina yoyote, kuchukua hatua kwa kiongozi yoyote wa serikali atakayebainika kuvuruga au kuhujumu shughuli za uchaguzi.
Alisema jukumu lingine ni kusimamia usalama wa nchi kupitia vyombo vya usalama na kutoa ulinzi unaostahiki katika mikutano ya kampeni na mikusanyiko yote iliyo rasmi ya vyama vya siasa.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi, Jaji Aziza Iddi Suwed, alisema ZEC imezingatia kifungu cha 65 cha sheria ya uchaguzi sheria namba nne ya mwaka 2018 kinachoelekeza kutayarishwa kanuni za maadili za kuongoza shughuli za vyama na wadau wengine katika uchaguzi.
Jaji Aziza, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ZEC, alisema kamati hiyo imepewa jukumu la kuandaa kanuni za maadili ya uchaguzi na kusimamia utekelezaji wake katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Alisema madhumuni ya kanuni hizo ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi, usawa katika ushindani na uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu kuzingatia misingi ya uhuru, haki na usawa.
Mwenyekiti huyo, alisema madhumuni mengine ni kuzingatia vigezo vya kikanda na kimataifa ya uchaguzi wa demokrasia.
Kwa mujibu wa kanuni ya 12, kila chama kinachoshiriki uchaguzi unaofanywa na ZEC, kinawajibika kutia saini maadili hayo, ambayo yatakuwa mwongozo na dira ya uendeshaji wa harakati za kampeni za uchaguzi wa uwazi, usawa, uadilifu na kuzingatia uwajibikaji kwa kila mshiriki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Uchaguzi, Thabit Idarous Faina, alisema tukio hilo ni kuashiria Zanzibar inaingia katika uchaguzi na kuhakikisha amani inatawala kipindi cha uchaguzi.
Dk. Islam Seif kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, alisema kanuni hizo ni kuashiria kwamba, amani inatawala kabla, wakati wa uchaguzi na kumalizika kwa upigaji kura.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya siasa, Ameir Hassan Ameir kutoka Chama Makini, alisema kwa niaba ya vyama vya siasa, wapo tayari kutii maadili hayo na imani yao, watatumia majukwaa kuzungumzia sera.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kuandika historia katika uchaguzi huo na kufuatilia sera za vyama vya siasa katika hali ya amani na utulivu.




